1. Jamani siwakemei, si uzuzu nayosema
Nisiposema ni hai, nitakosa yangu dhima
Nasema nikiwarai, mnelewe himahima
Ulevi gani ‘mezuka , mitandao kutuganda?
2 Uzuriwe haufichiki , kwote duniani nzima
Hunganisha halaiki , kukata nyingi gharama
Wambali hatahabiki , rahisi jumbe hutuma
Ila ulevi umezuka, mitandao ‘metuganda!
3 Wasichana wavulana, tuvutini hawatoki
Asubuhi na mchana, usiku na hawachoki
Baadhi wanayaona , kamwe hayaafikiki
Ulevi gani ‘mezuka ,mitandao kutuganda?
4 Mara pekee acheka , pole siwaiti fyatu
Ghafla aungulika, sababu sizo za kwetu
‘lipoona ya kucheka , ‘meyaona yaso utu
Ulevi gani ‘mezuka , mitandao kutuganda?
5 Utamuona kijana , kimya simu mkononi
Hataki kusemezana ,na wenzi yuko onlaini
Hata kama mwajuana , ‘takupuuza yakini
Ulevi gani ‘mezuka , mitandao kutuganda?
6 ‘kimuona yu njiani , kainamia simuni
Akanyagapo haoni, kama kipofu fulani
Wenzake hapo njiani , nusra gongwa komoni
Ulevi gani ‘mezuka , mitandao kutuganda?
7 Kuigana ni uwele , dhambi na uafkani
Mambo maovu ya kule , wengi wanayathamini
Waridhike na shule , wasioze ukubwani
Ulevi gani ‘mezuka ,mitandao kutuganda?
8. Huko wengi hawafai , kipata mpenzi chunga
Wapo walofika bei , kuumizwa kajiyonga
Thamini wako uhai , siri zako hebu funga
Ulevi gani ‘mezuka , mitandao kutuganda?
9 Sijasita sijachoka , ni mda umenitoka
Najua hujanichoka , mana sikuwa nabweka
Tuzikomeshe hakika, athari za kuungika
Ulevi gani ‘mezuka , mitandao kutuganda?
Shairi hili limetungwa na mbilA
Kazi nzuri kaka!
LikeLike