SIO PAMBO

LIMETUNGWA NA FADHILA MWANANGURA #MALENGA MWEMA

Nalikalia kigogo, niweze kulijadili
Hili neno sikidogo, linaniuma akili
Sitolilumba kidigo, Kuchengwa hilo kubali
Kuavya mimba si pambo, msi mwana ni mkiwa.

Sina hasira za mbogo, naidumisha asili
Hata mkazua zogo, sitouficha ukweli
Siuogopi mzigo, vyema nitaukabili.
Kuavya mimba si pambo, msi mwana ni mkiwa.


Ni wengi hutaka wana, japo wakuvirigiza
Wewe kakupa rabana, uhai wampoteza
Wauthamini ujana, molao unamkwaza
Kuavya mimba si pambo,msi mwana ni mkiwa.


Ungalitaka kutamba, nakukana uajuza
Ubaki bure mtamba, kizazi umekichuza
Ikose mwana na nyumba, nani atayekuweza
Kuavya mimba si pambo, msi mwana ni mkiwa.


Kuavya mama si pambo, aso mwana ni mkiwa
Boresha umbo si jambo, ila umtuhumiwa
Tembea kwa majigambo, kwa mola umelaniwa
Kuavya mimba si pambo, msi mwana ni mkiwa

Kupata mwana ni jambo, tena kubwa nawajuza
Wengine huenda ng’ambo kuitafuta miujiza
Mbona wahujumu tumbo, na mwana wampoteza
Kuavya mimba si pambo, msi mwana ni mkiwa.


Kuzaa dada ni nembo, ya heshima kuikweza
Silo dogo kwetu jambo, wazi ninawaeleza
Iweje ufanywe chambo, na wenzi wamle pweza
Kuavya mimba si pambo, msi mwana ni mkiwa.


Mwisho acheni mkumbo, mageni kuyaigiza
Msiyaige ya ng’ambo, ya vidonge kuvimeza
Nilosema si utumbo, Fadhili nawakataza
Kuavya mimba si pambo, msi mwana ni mkiwa.

Limetungwa na Fadhili Kalamu Mwanangura
#MALENGA MWEMA.

RAHA

Ubeti wa kwanza (1 )

Asali tamu ya guru , raha kutekerenyeka
Kupatiwa kwa uhuru, nafsi yanyong’onyeka
Hii haina ushuru , K.R.A yaumbuka
Mapenzi hasa Napewa , sikuiga ni kufana


Ubeti wa pili ( 2 )

jinsi alivyoumbika , mbila mi nala vinono
Kitabu nikiandika , kalamu haishi wino
Niruhusu kutamka , uzi mepata mshono
Mapenzi hasa napewa , sikuiga ni kufana


Ubeti wa tatu ( 3 )

Mwali kungwi wake nani , wote nimpelekee
Anayoyafanya honey, hataki nijichokee
Bembelezi kitandani , naimbiwa nipumbae
Mapenzi hasa napewa , si kuiga ni kufana

Ubeti wa nne ( 4 )

Sauti yake hayuni , nyororo si karipia
Akiwa yu ubavuni , taratibu aongea
Nahisi mbingu fulani , peponi nishaingia
Mapenzi hasa napewa , si kuiga ni kufana


Ubeti wa tano ( 5 )

Umbo limeniridhia , kama chupa ya fanta
Zote nyanja mekolea , kidari chapwetepweta
Guu la bia lakaa , nyuma rojo latokota
Mapenzi hasa napewa , si kuiga nikufana

Ubeti wa sita ( 6 )

Mapishi ayajulia , viungo navyoungia
Mwiko nalo sufuria , matumizi nasifia
Na hakuna kusalia , chakulache maridhia
Mapenzi hasa napewa , si kuiga nikufana


Ubeti wa saba ( 7 )

Ameninasa samaki , napumba nimesinyaa
Mwengine katu sitaki , tengani nimenasia
Kwaheri mlo wa kiki, nafunga zangu aua
Nenda pewa yangu haki , si kuiga ni kufana

Shairi limetungwa na mbilA

WENGINE

Ubeti wa kwanza ( 1 )

Hii nafasi nyingine , nudhumu kuiandika
Niseme neno lengine , kuihusu kila rika
Nikiyasaza mengine , bado hayajanifika
Mabinadamu mengine , jina ndo limebakia

Ubeti wa pili ( 2 )

Jina ndo limebakia , layasitiri mengine
Hawana hata ridhia , kiyaokoa mengine
Bure yakunyamazia , yakusengenya kwengine
Mabinadamu mengine , yakashifia mengine

Ubeti wa tatu ( 3 )

Yakashifia vyengine , japo kweli yaujua
Yataka picha nyengine , tena mbaya kuenea
Lengo lao si jengine, ni sifazo kuchafua
Mabinadamu mengine , roho zao zimefura


Ubeti wa nne ( 4 )

Roho zao zimefura , kisa choyo kwa wengine
Eti kwayo ni hasara , kuwakirimu wengine
Hatari kama kombora , mbona nyimana vyengine
Mabinadamu mengine , mbinguni hawana chao

Ubeti wa tano ( 5 )

Mbinguni hawana chao , labda pepo nyengine
Kuwalaumu wenzao , kwao kasoro nyingine
Wataka Utete nao , ndio furaha pengine
Mabinadamu mengine , Mungu pole yasamehe


Ubeti wa sita ( 6 )

Mungu pole yasemehe , yote makosa mengine
Na usia yachukue , yasiasi kivyengine
Nami huru mnachie , zangu shughuli zengine
Mabinadamu mengine , wao si watu pengine .

shairi hili limeandikwa na mbilA

NYONYO

Ubeti wa kwanza (1 )

Kwa wanaonisikia , ni shairi si waraka
Naghani najifutua , pwamu zinanichemka
La mama najinyonyea , lengine sitotosheka
Kiswahili aminia , nyonyoyo naitosheka


Ubeti wa pili ( 2 )

Zengine mi huongea , ila sipendi hakika
Mama nimemzoea , nimeishi kuridhika
Manenoye asilia , matamu pita mipaka
Kiswahili aminia , nyonyoyo naitosheka

Ubeti wa tatu ( 3 )

Nini hicho mwatambia ,kama si lugha tukuka
Lugha yenye asilia , mashariki Afrika
Kenya na tanga twongea , burundi rwanda yafika
Kiswahili aminia, nyonyoyo naitosheka

Ubeti wa nne ( 4)
Mwacha chake mepotea , fasihiye ni fanaka
Methalize nazijua , misemo losemezeka
Na Vitendawili pia , na mafumbo ninashika
Nahau nazijulia , mbona nende kupotoka

Ubeti wa tano ( 5 )
Tamati nikijitua , nawaita kuitika
Mje nyote kuongea , lugha tamu na tajika
Asia weze enea , bara yote kadhalika
Kiswahili aminia , nyonyoyo naitosheka

Shairi hili limetungwa na mbilA

POLE

1. Sijivishi uhakimu , uungu na ujuaji
Najitwika jukumu , kunena langu hitaji
Nahitaji ‘siwe ngumu , samehe na ufariji
Sema pole ukosapo , sema pole ukoswapo



2. Dunia hii ni moja , waliomo ndio wengi
Na ilivyojaa vihoja , utakosewa na vingi
Kwako usiwe na haja , kubeba vyote kwa wingi
Sema pole ukosapo , sema pole ukoswapo



3. Utaumia moyoni , ukiendekeza chuki
Weka toba rohoni , chuki mzazi wa dhiki
Usifungie kooni , zahama litabiriki
Sema pole ukosapo , sema pole ukoswapo



4. Mengine ni makusudi , akuudhi navyopenda
Mengine niya ahadi , kukumiza kukufyanda
Usitake kujinadi , we poa usijekonda
Sema pole ukosapo , sema pole ukoswapo


5. Hata kabla yafike, ukiona yaepuke
Katu usiangaike , kukabili uumbuke
Na ndovu msamba wake , ‘sishindane upasuke
Sema pole ukosapo , sema pole ukoswapo


6 Kuongea huliwaza , hutakatisha nafsi
Usiongee kuumiza , kulipizia kisasi
Ulimi funza kusaza , hicho ni kiungo hasi
Sema pole ukosapo , sema pole ukoswapo

7. Yako toba ndilo jibu , la kikwazo siku zote
Uongelee sababu , sio lengine lolote
kishasema kuwa bubu , sibishanie lolote
Sema pole ukosapo , sema pole ukoswapo.

8. Hapo mimi ninakoma , nikiongeza ‘takosa
Yote niliyoyasema , ndiyo yanayokupasa
vuliwa nguo chutama , ndio uungwana hasa
Sema pole ukosapo , sema pole ukoswapo.

Shairi hili limetungwa na mbilA

MITANDAO

1. Jamani siwakemei, si uzuzu nayosema
Nisiposema ni hai, nitakosa yangu dhima
Nasema nikiwarai, mnelewe himahima
Ulevi gani ‘mezuka , mitandao kutuganda?

2 Uzuriwe haufichiki , kwote duniani nzima
Hunganisha halaiki , kukata nyingi gharama
Wambali hatahabiki , rahisi jumbe hutuma
Ila ulevi umezuka, mitandao ‘metuganda!

3 Wasichana wavulana, tuvutini hawatoki
Asubuhi na mchana, usiku na hawachoki
Baadhi wanayaona , kamwe hayaafikiki
Ulevi gani ‘mezuka ,mitandao kutuganda?

4 Mara pekee acheka , pole siwaiti fyatu
Ghafla aungulika, sababu sizo za kwetu
‘lipoona ya kucheka , ‘meyaona yaso utu
Ulevi gani ‘mezuka , mitandao kutuganda?

5 Utamuona kijana , kimya simu mkononi
Hataki kusemezana ,na wenzi yuko onlaini
Hata kama mwajuana , ‘takupuuza yakini
Ulevi gani ‘mezuka , mitandao kutuganda?


6 ‘kimuona yu njiani , kainamia simuni
Akanyagapo haoni, kama kipofu fulani
Wenzake hapo njiani , nusra gongwa komoni
Ulevi gani ‘mezuka , mitandao kutuganda?

7 Kuigana ni uwele , dhambi na uafkani
Mambo maovu ya kule , wengi wanayathamini
Waridhike na shule , wasioze ukubwani
Ulevi gani ‘mezuka ,mitandao kutuganda?

8. Huko wengi hawafai , kipata mpenzi chunga
Wapo walofika bei , kuumizwa kajiyonga
Thamini wako uhai , siri zako hebu funga
Ulevi gani ‘mezuka , mitandao kutuganda?

9 Sijasita sijachoka , ni mda umenitoka
Najua hujanichoka , mana sikuwa nabweka
Tuzikomeshe hakika, athari za kuungika
Ulevi gani ‘mezuka , mitandao kutuganda?

Shairi hili limetungwa na mbilA