Ubeti wa kwanza ( 1 )
Hii nafasi nyingine , nudhumu kuiandika
Niseme neno lengine , kuihusu kila rika
Nikiyasaza mengine , bado hayajanifika
Mabinadamu mengine , jina ndo limebakia
Ubeti wa pili ( 2 )
Jina ndo limebakia , layasitiri mengine
Hawana hata ridhia , kiyaokoa mengine
Bure yakunyamazia , yakusengenya kwengine
Mabinadamu mengine , yakashifia mengine
Ubeti wa tatu ( 3 )
Yakashifia vyengine , japo kweli yaujua
Yataka picha nyengine , tena mbaya kuenea
Lengo lao si jengine, ni sifazo kuchafua
Mabinadamu mengine , roho zao zimefura
Ubeti wa nne ( 4 )
Roho zao zimefura , kisa choyo kwa wengine
Eti kwayo ni hasara , kuwakirimu wengine
Hatari kama kombora , mbona nyimana vyengine
Mabinadamu mengine , mbinguni hawana chao
Ubeti wa tano ( 5 )
Mbinguni hawana chao , labda pepo nyengine
Kuwalaumu wenzao , kwao kasoro nyingine
Wataka Utete nao , ndio furaha pengine
Mabinadamu mengine , Mungu pole yasamehe
Ubeti wa sita ( 6 )
Mungu pole yasemehe , yote makosa mengine
Na usia yachukue , yasiasi kivyengine
Nami huru mnachie , zangu shughuli zengine
Mabinadamu mengine , wao si watu pengine .
shairi hili limeandikwa na mbilA