SIO PAMBO

LIMETUNGWA NA FADHILA MWANANGURA #MALENGA MWEMA

Nalikalia kigogo, niweze kulijadili
Hili neno sikidogo, linaniuma akili
Sitolilumba kidigo, Kuchengwa hilo kubali
Kuavya mimba si pambo, msi mwana ni mkiwa.

Sina hasira za mbogo, naidumisha asili
Hata mkazua zogo, sitouficha ukweli
Siuogopi mzigo, vyema nitaukabili.
Kuavya mimba si pambo, msi mwana ni mkiwa.


Ni wengi hutaka wana, japo wakuvirigiza
Wewe kakupa rabana, uhai wampoteza
Wauthamini ujana, molao unamkwaza
Kuavya mimba si pambo,msi mwana ni mkiwa.


Ungalitaka kutamba, nakukana uajuza
Ubaki bure mtamba, kizazi umekichuza
Ikose mwana na nyumba, nani atayekuweza
Kuavya mimba si pambo, msi mwana ni mkiwa.


Kuavya mama si pambo, aso mwana ni mkiwa
Boresha umbo si jambo, ila umtuhumiwa
Tembea kwa majigambo, kwa mola umelaniwa
Kuavya mimba si pambo, msi mwana ni mkiwa

Kupata mwana ni jambo, tena kubwa nawajuza
Wengine huenda ng’ambo kuitafuta miujiza
Mbona wahujumu tumbo, na mwana wampoteza
Kuavya mimba si pambo, msi mwana ni mkiwa.


Kuzaa dada ni nembo, ya heshima kuikweza
Silo dogo kwetu jambo, wazi ninawaeleza
Iweje ufanywe chambo, na wenzi wamle pweza
Kuavya mimba si pambo, msi mwana ni mkiwa.


Mwisho acheni mkumbo, mageni kuyaigiza
Msiyaige ya ng’ambo, ya vidonge kuvimeza
Nilosema si utumbo, Fadhili nawakataza
Kuavya mimba si pambo, msi mwana ni mkiwa.

Limetungwa na Fadhili Kalamu Mwanangura
#MALENGA MWEMA.

Leave a Comment